Pwani yang'ara kwa miradi mipya

TANZANIA ya viwanda ni ndoto ambayo haina muda mrefu itatimizwa baada ya mwelekeo wa kujenga uchumi wa viwanda kuanza kuwa mzuri, na huku mifuko ya hifadhi ya jamii ikionesha nia ya kuwekeza katika miradi ya viwanda katika maeneo mbalimbali nchini.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema miradi ya viwanda mbalimbali imeanzishwa kutokana na mchango wa sekta binafsi katika mikoa mbalimbali nchini. Dk Mpango alikuwa akiwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka 2017/18.
Alisema kwa mfano, Mkoa wa Pwani una jumla ya miradi mipya ya viwanda 82. Aliitaja baadhi ya miradi mikubwa ya viwanda iliyozinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi kwa mkoa wa Pwani pekee ni viwanda viwili vya Tywford Tiles (Chalinze) na Goodwill Ceramic (Mkuranga) vya kutengeneza marumaru (tiles); kiwanda cha nondo cha Kiluwa Steel Industries Ltd (Mlandizi Pwani) ambacho kimeanza uzalishaji; kiwanda cha Global Packaging (Mailimoja Pwani) ambacho kinafanya kazi.
Vingine ni kiwanda cha kutengeneza juisi ya matunda cha Bakhresa Food Product Ltd (Mkuranga) ambacho kimezinduliwa na kinafanya kazi; kiwanda cha Elyven Agric Co. Ltd (Bagamoyo); kiwanda cha juisi cha Sayona Fruits Ltd (Mboga Pwani); na kiwanda cha KEDS Tanzania Co. Ltd (Kibaha Pwani).
Alieleza kuwa serikali imekuwa na mchango mkubwa kuwezesha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda hivi, ikiwamo kusaidia upatikanaji wa ardhi, kuweka miundombinu inayohitajika, na kutoa vibali vya ujenzi na pia vivutio. Aidha, alieleza kuwa serikali pia kupitia mashirika yake mbalimbali imeanza kuwekeza katika ujenzi wa viwanda.
Alisema mwitikio wa pekee na wa kupongezwa ni wa mifuko ya hifadhi ya Jamii, ambapo PPF na NSSF wanashirikiana kuwekeza katika kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari katika eneo la Mkulazi na Mbigiri (Morogoro); na LAPF wanajenga machinjio ya kisasa ya nyama (kwa Makunganya – Morogoro).
“Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) linashirikiana na sekta binafsi kwa ajili ya uwekezaji katika eneo la viwanda la TAMCO – Kibaha kwa uendelezaji wa viwanda vya nguo na uunganishaji wa magari na matrekta, ambapo kiwanda cha kuunganisha matrekta kimefikia hatua ya kuanza majaribio.
“Hatua nyingine zinazoendelea chini ya NDC ni pamoja na jitihada za kufufua Kiwanda cha General Tyre (Arusha); hatua za awali za uwekezaji katika mradi wa uchenjuaji wa Magadi Soda (Bonde la Engaruka). NDC pia kwa ubia na kampuni ya TCIMRL ya China imewekeza katika miradi ya Mchuchuma na Liganga,” alisema Dk Mpango.
Aliitaja baadhi ya miradi inayotarajiwa kutekelezwa na mifuko hiyo katika mwaka 2017/18 ni pamoja na ufufuaji wa kiwanda cha sukari katika Gereza la Mbigiri Dakawa Morogoro; kiwanda cha kutengeneza viatu katika Gereza la Karanga Moshi; kiwanda cha nguo cha Urafiki; Dar es Salaam; kiwanda cha Morogoro Canvas Mill.
Miradi mingine ni kiwanda cha chai cha Mponde kilichopo Lushoto mkoani Tanga; kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools (KMTC) na kiwanda cha Kubangua Korosho cha Tandahimba na Newala.
“Vile vile, mifuko hii inatarajia kuanzisha viwanda vipya katika maeneo mbalimbali, vikiwemo: kiwanda cha dawa; kiwanda cha kuzalisha bidhaa za hospitali na gesi ya oksijeni; kiwanda cha kusindika zabibu, Chinangali Dodoma; viwanda vya kusindika nafaka na ukamuaji wa mafuta; na kiwanda cha kuzalisha wanga kutokana na zao la muhogo na viazi vitamu huko Lindi,” alieleza.
Kuhusu kihatarishi vinavyoweza kuathiri utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa, alikitaja kikwazo kikuu cha ndani ni ufinyu wa rasilimali fedha na uwepo wa tofauti za mpangilio wa vipaumbele, mpango- kazi na mtiririko wa upatikanaji fedha baina ya taasisi za utekelezaji.
Kuhusu ugharamiaji wa mpango, alisema katika mwaka 2017/18, Sh trilioni 11.99 zimetengwa kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kati ya hizo, alisema Sh trilioni 8.96 ni fedha za ndani na Sh trilioni 3.02 ni fedha za nje.
“Hivyo, fedha zilizotengwa katika bajeti ya maendeleo zimeongezeka kutoka Sh bilioni 11,820.5 mwaka 2016/17 hadi Sh bilioni 11,999.6 kwa mwaka 2017/18, ikiwa ni sawa na asilimia 38 ya bajeti yote.
“Kiasi hiki ni kikubwa kwa asilimia 1.2 ya makadirio ya kutenga Shilingi bilioni 11.80 kila mwaka kutoka mapato ya Serikali kama ilivyojidhihirisha katika mapitio ya utekelezaji kwa mwaka 2016/17,” alieleza Dk Mpango.
Alisema serikali itahakikisha kuwa kiasi cha fedha kilichopangwa kwa matumizi ya maendeleo kinapatikana na kugawiwa kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo iliyokusudiwa na kwa wakati.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Baada ya Kumwagana na Ali Kiba,,Jokate Aaamua Kuweka Wazi Vigezo kwa Kidume Mwingine Anayemtaka..!!!

Mimi Mars Amkana Dada Ake Vanessa Mdee...Asema....